top of page

SISI NI NANI?

Kanisa la Biblia Publishers ni idara ya Maandiko ya Kanisa la Biblia Tanzania. 

KAZI YETU

Kazi yetu ni kutafsiri, kuandaa na kutoa maelezo ya Biblia kwa Kiswahili. Lengo letu ni kutoa vitabu ili watu wapate kufahamu Biblia vizuri zaidi, wakiishaelewa wenyewe wawafundishe wengine Neno la Mungu na kutafsiri maana yake kwa maisha ya kila siku. 

newbooks.jpg
mbb-seminar.jpg

DHAMIRA YETU

Kanisa la Biblia Publishers inadhamiria kukuza ufahamu wa Biblia Afrika Mashariki kwa njia ya kusambaza maandiko ya Kikristo yanayosaidia kuelewa Maandiko kwa manufaa binafsi, ili kukua kiroho. Pia maandiko yetu yanatumika katika vyuo vya Biblia kama vitabu vya rejea vya Kiswahili.

HISTORIA YA KLB PUBLISHERS

1980

Vitabu vya kwanza „Panorama ya Biblia“ na „Imani yetu Ndiyo Ushindi“ vilitolewa mwaka 1980 na kuchapishwa na Nusch-Druck Gummersbach, Ujerumani. Vitabu vyote viwili vilitafsiriwa kutoka Kijerumani na Helmut Gräf, aliyekuwa mwanzilishi wa Chuo cha Biblia Nanjoka, Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, Tanzania. Palikuwa na uhitaji wa kuandika au kutafsiri vitabu vinavyoeleza Biblia kwa walimu na wanafunzi wa Biblia Afrika Mashariki. 

1986

Kisha Helmut Gräf alianza kutafsiri ufafanuzi wa Agano Jipya katika vitabu 5 vinavyoitwa “Agano Jipya Lasema” No. 1 hadi 5, na badaye aliongeza vitabu 10 vya “Agano la Kale Lasema” No. 1 hadi 10. Huu ni ufafanuzi wa kwanza wa Kiswahili wa Biblia nzima. Mfululizo una vitabu 15 na ulitolewa mwaka 1986 hadi 1990. Badaye vitabu vyote 15 vilijumlishwa katika kitabu kimoja kinene kinachoitwa “Bibla Inasema” na kutolewa mwaka 2000 Dodoma. 

1991

Kazi ya kusambaza vitabu haikuwa rahisi kutoka Tunduru, upande wa kusini mwa Tanzania. Kwa hiyo kituo cha maandiko Kanisa la Biblia Publishers na Emmaus kilianza kujenga kuanzia mwaka 1991. Baada ya kuhamia mji mkuu wa Tanzania Dodoma, katikati ya nchi, usambazaji uliendelea vizuri zaidi kuanzia mwaka 1993.

1995

Wakati wa ujenzi wa kituo cha maandiko Dodoma kuanzia mwaka 1991 Nd Helmut Gräf aliendelea kutafsiri “Kamusi ya Biblia” kutoka Kiingereza. Kitabu hiki muhimu cha rejea kilichoandikwa na Don Fleming kilitolewa Dodoma mwaka 1995. Kisha alijumlisha vitabu vidogo 15 “Agano la Kale Lasema” na “Agano Jipya Lasema” kuviweka katika kitabu kimoja “Biblia Inasema” kilichotolewa mwaka 2000.

2003

Hatua nyingine kubwa ilikuwa kutafsiri na kutoa vitabu viwili vya Erich Sauer kutoka Kijerumani kuhusu historia ya wokovu. Vitabu viwili “The Dawn of World Redemption” na “The Triumph of the Crucified” vilitolewa mwaka 2003 katika kitabu kimoja kinachoitwa “Ufunuo wa Mungu na Itikio la Imani.” Kwa kutumia kitabu hiki msomaji wa “Panorama ya Biblia” ataelewa vizuri zaidi historia ya Mungu na wanadamu. 

2011

Mwaka 2011 kwa mara ya kwanza tulitoa kitabu cha watoto wadogo “Biblia ya kupaka rangi” ili wazazi wawasomee watoto habari za Biblia au watoto wajisomee wenyewe na kuchora picha kwa penseli za rangi. Badaye (2012 – 2016) tulikuwa tumeendelea kutoa masomo ya kufundisha watoto kanisani au mashuleni. Mfululizo huu unaitwa “Masomo Bunifu ya Biblia” na ina vitabu na picha zake kwa mwalimu anayefundisha watoto wenye umri wa miaka 4 – 12 katika rika 3, jumla seti zipo 16.

2019

Tunaendelea kuandaa mfululizo mpya wa maelezo ya Biblia ya William MacDonald “Ufafanuzi Hai wa Biblia kwa Maisha ya Kiroho.” Mwishoni kutakuwa na juzuu 8. Tumeshaanza kutoa vitabu 4 vya Agano Jipya kwa kutoa Vol. 1 mwaka 2019. Biblia inaelezwa mstari hadi mstari kwa kufuata Biblia Union Version iliyoboreshwa.  Tafsiri zingine kama Habari Njema, Roehl, Neno na Biblia ya Kiafrika zinatumika pia ili kuonesha maana ya lugha ya asili. 

2022

Umuhimu wa kujitangaza katika mitandao ya jamii umetusukuma sana kujikita katika uwanja huu. Kwa hiyo sasa tunaendelea kujitangaza kwa kupitia tovuti, whatsapp na Instagram.

bottom of page